Tuesday 21 June 2011

FASIHI SIMULIZI

UTANGULIZI


Sanaa ni ufundi wa hali ya juu wa kuwasilisha mawazo kwa njia inayoathiri. Kutegemea nyenzo ya uwasilishi, tuna aina zifuatazo za sanaa:

Nyenzo
Sanaa
Rangi
Uchoraji
Nyuzi
Ufumaji/ Udarizi
Miti/ mawe
Uchongaji
Towe
Ufinyanzi
Lahani
Muziki
Lugha
Fasihi

MAANA YA FASIHI

Ni sanaa ya lugha iwasilishayo tajiriba zinazomwathiri binadamu. Misingi ya fasihi huwa katika ubunifu wa kuteua, kupanga na kunakidi tajiriba mbalimbali za maisha.
Fasihi kama dhana, imeelezwa na wengi kwa kuegemea nadharia na mitazamo mbali mbali. Hata hivyo ni muhimu tufahamu ya kwamba maana inayopewa dhana au kitu fulani, huchukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu wanaohusika, mahali dhana hiyo inamotokea, na hata kipindi au wakati husika. Hii ndiyo sababu twapata maana mbalimbali zikitolewa kuhusu fasihi. Kwa mfano, waandishi wengi wa Kimagharibi wamesisitiza kwamba fasihi yahusu tu kazi zilizoandikwa. Ndiposa Okot P' Bitek (1973:18) anasema:
Katika usomi wa kimagharibi, fasihi humaanisha maandishi ya wakati au nchi fulani, hasa ile yenye kupewa thamani ya juu katika mtindo na uendelezaji wake. Ufafanuzi huu unaotilia mkazo uandishi walenga kueleza kwamba fasihi ni amali ya jamii zilizovumbua sanaa ya uandishi.
Kwa hivyo, fasihi, kulingana na mtizamo huo wa kimagharibi, imechukuana na uandishi, na hivyo basi fasihi si fasihi hadi iandikwe. Bila shaka mtazamo kama huu hupuuza fasihi-simulizi. Ama kwa hakika hiyo hatua ya kuihusisha fasihi na maandishi ni ya maksuudi inayodhamiriwa kuonyesha fasihi kama amali ya jamii yenye taluma ya kusoma na kuandika. Ni kile kitendo cha kibinafsi au cha kubagua ambacho hudhamiria kuonyesha jamii ambazo hazina taaluma ya uandishi kama jamii duni.

Ukweli ni kwamba pamewahi kuwepo na bado zipo kazi za fasihi za hali ya juu kutoka kwa jamii ambazo hazikuwa na taaluma ya kusoma na kuandika. Isitoshe, pana mifano mingi ya kazi zilizokuwa katika masimulizi hapo awali, lakini sasa zimehifadhika katika maandishi na huratibiwa kama kazi za fasihi. Kazi nyingi za ushairi wa Kiswahili ni mifano ya kazi kama hizo. P'Bitek (1973:20) kwa kuipinga kauli ya kutengea fasihi jamii fulani anasema;
Tunashurutika kukataa ufafanuzi huu unaotenga na kubagua; na badala yake kuunda ufafanuzi wa kimapinduzi utakaoionyesha fasihi kama inayochukua kazi zote za kubuniwa za wanadamu zinazoelezwa kwa maneno.
Maneno haya ya P’Bitek ni maneno ya kuvutia lakini huenda yasiwe na dharura yoyote katika wakati huu maana pana kazi kemkem za fasihi katika tamaduni zetu ambazo wakati wa awali hazingeorodheshwa kama kazi za fasihi. Lakini bado hatujatoa mwongozo thabiti wa kuonyesha ni kazi zipi zinaratibiwa kama za fasihi na ni zipi zinazoingia katika kikundi kingine.

Waandishi wengi wameandika kuhusu swala hili la fasihi, na maoni yao huwa kwa njia moja au nyengine yanadhihirisha kutotosheka kwao na yaliyosemwa na wengine kuhusu swala hilo, wengine wakijaribu kubainisha utunzi uliopo, na wengine wakifafanua zaidi maelezo yaliyopo. P’Bitek (kama hapo juu)  anazidi kusema; Fasihi husimamia kazi zote bunifu anazozitumia mwanadamu kujieleza kwa maneno ambayo yaweza kuimbwa, kusemwa, au kuandikwa. Ameir Issa Haji (1983:30) anasema kuwa fasihi ni:
Sanaa itumiayo maneno ili kutoa picha halisi ya mwanadamu akiwa maishani mwake; mahusiano yake na viumbe wengine, migogoro yake na mazingira, shida zake, raha zake, matumaini yake na jinsi anavyopiga hatua katika maendeleo yake.
Mtizamo kama huu waitazama fasihi kama kazi inayoendelezwa kwa maneno, iwe andishi au simulizi [kuandika na kusimulia ni mtambo tu wa kuiwasilisha kazi hiyo]. Kuandika sawa na kuchonga au kuchora ni njia ya kueleza dhana tu, na jinsi ambavyo mchoraji hutumia rangi katika kazi yake, mtunzi wa kazi ya fasihi hutumia maneno kueleza dhana na hisia zake. Maneno hayo huenda akayaandika, akayaimba au akayazungumza. Kwa hivyo, fasihi iwe imeandikwa au imesimuliwa bado ni fasihi.

Naye Odaga (1985:xxi) anasema kwamba; Fasihi ni sanaa ambayo mtambo wake ni neno na kiini chake ni binadamu. Toleo la kumi na nne la Compton’s Encyclopedia (1974:305) yaeleza fasihi kwa njia pana huku fasihi ikichuliwa kama; iliyo zaidi ya lugha. Ni dhana na hisia zilizovingikwa katika muziki wa lugha. Na huchukua umbo la maneno na picha zilizowekwa pamoja na ubunifu. Fasihi ni jinsi ya kuona, kuhisi, kufahamu.

Kwa muhtasari twaweza kusema kwamba pana kauli hizi za kimsingi ambazo hujitokeza katika fafanuzi za wataalam hawa na wengine wengi kuhusu dhana ya fasihi:
·         Fasihi ni sanaa inayodhihiri ubunifu
·         inayotumia maneno kuwasilisha mambo yake
·         hulenga binadamu kama kiini chake
Kama tulivyotaja hapo awali maana ya neno au dhana yoyote hutegemea mambo mengi na hivyo basi fasili hii yetu ya fasihi huenda isichukuane na maoni ya mwingine anayechagua kuitazama fasihi kwa njia tofauti. Lakini hata mhakiki atumie mtizamo gani, fasili yake pamoja na hitimisho lake litategemea anachukua fasihi kumaanisha nini pamoja na jukumu la mtunzi wa fasihi hiyo. Katika misingi hii, huenda likawa jambo mwafaka kuzingatia baadhi ya vigezo vilivyowahi kutumiwa katika kufafanua fasihi ili tupate msingi wa kufanya uhakiki.

Pametokea vigezo tofauti vya kuifafanua fasihi kutegemea msisitizo anaotaka kuweka mfasili pamoja na maendeleo na mabadiliko ya maisha kihistoria. Kuna wale wanaosisitiza umbo la nje la fasihi ambao wamekita nadharia zao katika muundo huo ilhali wengine wanasisitiza umbo lake la ndani. Pana wale wanaochagua kuzingatia wahusika katika kutungwa kwa kazi hiyo, yaani mtunzi, hadhira yake na hata athari za jamii. Ndiposa twapata vigezo vilivyotumiwa ama vyalenga maumbo ya fasihi, maudhui yake au yote mawili.

Ni muhimu kueleza kwamba hivi vigezo tutakavyovitaja hapa, mara nyingi vimejitokeza katika utanzu wa uhakiki, hivi kwamba maelezo ya 'fasihi ni nini' yanatumiwa kutathimini kutimizika kwa masharti yanayozingatiwa na mtunzi anapotunga kazi yake. Kwa hivyo kama utunzi wa fasihi husisitiza maudhui mbali mbali basi huenda mhakiki akatumia kigezo hicho hicho katika kazi yake ya uhakiki kubainisha kufaulu kwa kazi hiyo katika lengo hilo.

Fasihi kama Sanaa Itumiayo Maneno
Aghalabu, wataalamu wametumia kigezo cha `neno' kama njia ya kutofautisha fasihi na sanaa nyingine kama vile uchoraji na uchongaji. Wanasema kwamba fasihi ni sanaa inayotumia maneno ili kuwasilisha maudhui na hoja zake. Wataalamu wanaoshikilia kigezo hiki ni wale wanaopinga kauli ya kimagharibi ya kuhusisha fasihi na taaluma ya maandishi.

Kwa hivyo, tunaposema kwamba fasihi ni sanaa inayotumia maneno huwa tayari tumeliacha wazi swala kuhusu maneno yaliyoandikwa au yaliyosimuliwa. Neno, liwe limeandikwa au limetamkwa, ni neno. Lakini sio kila neno huenda likaorodheshwa kama fasihi. Fasihi huwasilishwa kwa maneno lakini maneno hayo hutumiwa kwa njia maalum ili kuyatenganisha na maneno ya kawaida. Kwa hivyo lazima pawe na sura maalum zinazounda maneno ya fasihi ili kuyatofautisha na maneno ya kawaida. Ili kujitandua kutoka utata huu, ni muhimu kuichukulia fasihi sio kama maneno bali kama sanaa itumiayo maneno. Na matumizi ya maneno hayo katika fasihi huashiria usanii wa namna fulani. Usanii huo ndio unaofanya maneno ya fasihi yawe tofauti na maneno ya kawaida japo mofolojia na fonolojia yake ni sawa. Maneno yanayotumiwa katika fasihi ni maneno zaidi ya maneno mengine kwani yanatumiwa kisanaa. Lakini hamna maneno maalum yaliyotengewa fasihi na ambayo hayapatikani katika utanzu mwingine wowote wa maisha ya jamii. Ukweli ni kwamba katika fasihi, maneno ya kawaida hutumiwa kisanaa.

Kirumbi P.S (1975:10) anatutolea mfano wa jinsi maneno yanaweza kutumiwa kisanaa. Ametutolea mifano miwili ya shukrani zilizotolewa na watu wawili tofauti;
wa kwanza anasema:
Ndungu mpenzi,
Nimepokea msaada wako nami umenisaidia sana sikutazamia kupata msaada katika shida hii iliyonikuta. Ama Mungu mkubwa. Ndugu, asante sana kwa msaada wako. Kwa kweli nakushuru sana tena sana.
Mungu akubariki.

wa pili naye anasema:
Ndugu,
Sijasikia mkono ukipewa shukrani na mguu kwa kuutoa mwiba - lakini ni ujinga wa mguu kufikiria unastahili kutolewa mwiba, maana kuna miili isiyo na mikono, na miguu hiyo ichomwapo na miiba hutaabika sana. Hivyo sioni kustahili kwangu bali ni rehema na neema kuwa na ndugu, nami nimepata na kujifunza zaidi upendo wako.

Watu hawa wawili wametendewa jambo la kuwafaa na wote wametumia maneno kutoa shukrani zao. Hata ingawa ujumbe wa maneno yao ni mmoja, twaona kuwa maneno ya mmoja ni ya kisanaa ilhali ya mwingine ni ya kawaida. Maneno hayo yanapatikana katika msamiati wa jamii husika lakini jinsi yalivyoteuliwa na kutumiwa ndipo tofauti inatokea. Katika mfano wa pili kwa mfano, mtunzi anachagua kufananisha kitendo alichotendewa na ndugu yake na kitendo cha mkono kuondoa mwiba mguuni. Mguu unapochomwa ni mwiba huumia na huhitaji kuondelewa (kusaidiwa), kwani hauwezi kujitoa mwiba ule wenyewe. Hivyo ndivyo ilivyo katika fasihi; kwamba maneno hutumiwa kwa njia maalum (ya kisanaa) inayotoa mguso fulani kwa hadhira.

Wakati mwingine kazi ya fasihi huweza kuendelezwa kwa matendo badala ya maneno. Kwa mfano tamthilia huhusisha maneno na matendo pamoja ili kuwa kamili. Bila matendo, tamthilia haijakamilika. Kwa hivyo huenda maneno yakawa nguzo moja tu ya fasihi na kama sivyo, tamthilia itaachwa nje ya fasili ya fasihi. Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba hata hayo matendo katika tamthilia huweza kueleweka katika misingi ya maneno. Kwa hivyo kiini cha fasihi ni maneno. Na maneno hayo yanatumiwa kisanaa.

Fasihi kama Sanaa: Nadharia ya Umithilishaji
Njia moja ambayo pengine ni kongwe sana na iliyopata kutumiwa kufafanua fasihi kama sanaa ni ile ya kuiona fasihi kama aina ya umithilishaji. Kwa mtazamo huu, fasihi hufafanuliwa katika uhusiano wake na maisha; kwa kuiona kama njia ya kujenga tena au kuhuisha tukio au hali fulani ya maisha kwa kutumia mchoro na rangi. Huu ni mtizamo ulioendelezwa na Aristotle na kufuatiliwa na wafuasi wake. Abrams M.H (1981) anasema hivi kuhusu umthilishaji;
Katika kazi yake ya `Poetics', Aristotle anaeleza ushairi kama umithilishaji wa vitendo vya mwanadamu. Kwa `umithilishi' anamaanisha `uwakilishi', kwa msingi yake.
Kwa hivyo kwa maoni ya Aristotle, shairi humithilisha kwa kuchukua kitendo fulani cha mwanadamu na kukionyesha upya katika `mtambo' mpya - ule wa maneno.

Mtizamo huu wa kuiona fasihi kama sanaa ya umithilishaji waweza kufasiriwa kwa njia mbili kuu; kwanza, twaweza kuuchukulia kijuujuu na kupendekeza kwamba fasihi hujaribu kuiga na kumithilisha maisha; yaani maudhui ya fasihi ni tajiriba za watu waishio. Lakini pendekezo kama hili lazua matatizo kwani hatusemi mengi kuhusu fasihi kwa vile hatutilii maanani kile kinachofanyiwa hayo maudhui. Pia kwa kutumia neno `maisha' twaweza kuuchukulia kijuujuu na kupendekeza kwamba fasihi ni tajiriba za watu waishio. Pia kwa kutumia neno `maisha' twazua utata mkubwa kwani maisha ni kitu tofauti kwa watu tofauti kwani kila mmoja japo wanishi katika mazingira sawa, aghalabu huguswa na mambo kwa njia tofauti. Pili, twaweza kusema kwamba maisha yanaigwa kwa njia ambayo yanaumbwa upya na kutafsiriwa upya kwani hapawezekani kuondoa kitu kutoka mtambo mmoja na kukiingiza katika mtambo mwingine bila kukiadhiri au kukibadilisha. Dhana hii ya pili inakaribiana na mojawapo ya sura muhimu katika fasihi; ile ya kwamba malighafi ya fasihi huundwa upya na hata kubadilishwa. Lakini bado hatuonyeshi ni mambo gani ya maisha humithilishwa. Kuhusiana na hali hii Wellek na Warren (1949:95) wanasema;
Iwapo inachukuliwa kwamba fasihi, kwa wakati wowote ule, humulika hali ya kijamii iliyopo kwa uhalisi wake, basi hiyo si kweli; ni wazi, vile vile, kwamba si kweli kusema fasihi hudhihirisha baadhi ya uhalisi uliopo katika jamii.
Kwa hiyo, kwa maoni ya wataalamu hawa wawili kauli ya kuiona fasihi kama umithilishaji wa maisha ni ya kupotosha. Wanaendelea kutaja kwamba;
Fasihi kwa hakika si picha ya mkondo wa maisha, bali ni ufupisho na muhtasari wa historia nzima.
Wanalosisitiza hapa ni kwamba fasihi si picha ya moja kwa moja ya maisha bali ni muhtasari wa maisha na matukio yake. Lakini na wao hawatuelezi ni vipi fasihi yatofautiana na kumbukumbu iliyoandikwa kuhusu maisha na mwanahistoria. Ni kwamba kazi ya fasihi huzingatia kaida maalum zinazotawala kila utanzu wa fasihi na kuibainisha na kazi ya mwandishi wa historia kwa mfano.

Hata hiyo Wellek na Warren (1949:102) wanakiri kwamba, “hatuwezi kupuuza wazo kwamba picha fulani ya maisha huweza kupatikana katika fasihi.”
Pana kauli moja ambayo yajitokeza katika kigezo hiki cha kuiona fasihi kama sanaa inayomithilisha maisha. Katika umithilishi huu mtunzi anatumia maneno. Lakini katika dhana hii ingawa yasemekana kwamba fasihi huhusu maisha, hatuambiwi ni kwa kiwango gani. Hata hivyo mfumo huu unaotokana na nadharia ya umithilishaji umekuwa nguzo kwa kazi nyingi za fasihi na zisizo za fasihi. Abrams, M.H (1981) anasema;
Hata ingawa nadharia ya umithilishaji ilififia, ilichukuliwa tena ni R.S Crane na wahakiki wengine wa Chicago waliotumia misingi ya kiaristotle katika tathimini zao. Wahakiki wengi wa ki-marx huiona fasihi kama umithilishaji.
Kwa hivyo hata ingawa pana wale wanaopinga kuwa fasihi ni umithilishaji, kauli hii inatoa nguzo kwa mitizamo mingine kuhusu fasihi. Twaweza kusema kwamba pana uhusiano mkubwa kati ya umithilishaji na uhalisia (jambo ambalo huhimizwa sana katika baadhi ya kazi muhimu za fasihi).

Kazi nyingi za fasihi huweza kuhusishwa na umithilishaji. Methali na vitendawili ni tanzu za fasihi simulizi ambazo zinatumiwa sana na jamii kwa shughuli mbali mbali. Twapata kwa hakika kwamba jinsi methali zilivyo ni mfano halisi wa umithilishaji kwani dhana inayosimamiwa na methali huwakilisha hali halisi ya maisha. Maneno yanayojenga methali, vitendawili na hata misemo ni mfano wa aina fulani ya umithilishaji. Methali kama vile `mwamba ngoma ngozi huivutia kwake' imeundwa kama mithili ya moja kwa moja ya maisha ya mwanadamu. Kwamba mtu anapovuta ngozi wakati anapounda ngoma huwa anaivutia upande wake, (huo ni ukweli wa mambo) na hawezi kuivuta ikaendea mwenzake kwani itapuuza dhana ya kuvuta. Kwa hivyo kiini cha methali hii ni ukweli halisi wa mambo. Hivyo basi pana hali ya umithilishaji katika utanzu huo wa fasihi.

Kwa jumla twaona kwamba fasihi ni sanaa inayomithilisha. Umithilishaji huu hata hivyo si wa moja kwa moja kwani kama ingekuwa hivyo, basi hapangekuwa na tofauti kati ya fasihi na historia. Hapo ndipo twaingilia kigezo cha tatu cha kuieleza fasihi.

Dhana ya Ubunilizi
Hata ingawa kazi ya fasihi kwa kawaida huwa yamithilisha au kujaribu kuumba upya maisha kwa njia moja au nyengine, twatambua ukweli kwamba yaliyotungwa si maisha halisi moja kwa moja. Kwa mtizamo huu yaelekea kwamba fasihi si maisha halisi bali ni tokeo la ubunifu wa mtunzi ambao haukanganyi hali halisi ya maisha. Hata hivyo, ubunifu huu lazima uongozwe na kaida za hali halisi ya maisha yaani kama asemavyo Horace (1975:103):
Chochote utakachochagua kwa minajili ya kupendeza, hakikisha kwamba kipo karibu na ukweli.
Yaani mtunzi anapaswa kuufanya ulimwengu wake wa kubuni kuwa picha halisi ya maisha katika ukamilifu na ukweli wake, hata ingawa alivyoyashughulikia ni ya kubuni tu. Horace (1975:95) anafafanua zaidi kauli hii asemapo kwamba;
Washairi na wachoraji wamekuwa wakifurahia uhuru wa utunzi na kufanya majaribio jinsi watakavyo. Hili nalifahamu, na mimi kama mshairi hufurahia uhuru huo; lakini si kwa kiwango ambacho kwacho viumbe visivyotangamana vinawekwa pamoja, hivi kwamba ndege na nyoka wanawekwa pamoja, wanakondoo pamoja na simba marara.
Anachosisitiza Horace ni kuwa, hatuwezi kumnyima mtunzi uhuru wa kubuni, lakini mtunzi akumbuke kwamba ubunifu wake usikiuke kaida zinazotawala maisha halisi ya jamii. Kumpa mtunzi uhuru wa ubunifu na kisha umtarajie afuate kaida fulani ni kumnyima uhuru kamili. Kama mtunzi atakanganya hali halisi ya maisha kama mbinu yake ya kutunga, basi na tumpe uhuru huo alimradi kazi yake twaielewa kwa mtazamo huo. Kwa hivyo, fasihi si kazi inayohusu mambo ya kipekee bali ni uwasilishaji wa maisha ya jamii kwa njia bunifu isiyo ya moja kwa moja. Ndiposa Aristotle (1975:103) anasema:
Ni wazi kwamba, si jukumu la mshairi kuendeleza yaliyotokea bali huendeleza yanayoweza kutokea-yaani kinachoweza kutokea katika msingi ya haja au uwezekano.
Hapo ndipo fasihi hutofautiana na historia kwani wakati fasihi huendeleza linaloweza kutokea, historia huendeleza kilichotokea; na fasihi ikieleza lililotokea hulieleza kisanaa, sio moja kwa moja. Hivyo basi, fasihi ni utanzu unaoendeleza maisha kwa njia bunifu iliyojikita katika msingi na kaida zinazotawala maisha halisi.

Dhana ya Muundo
Ili kueleza maana ya fasihi, wataalamu wengi wamejaribu kuzingatia baadhi ya vigezo vinavyoitambulisha, hasa ikiwekwa katika mkabala mmoja na tanzu nyengine za maisha ya jamii. Twaweza kusema kwamba dhana ya ubunilizi ni njia nzuri ya kutofautisha fasihi na uhalisia pamoja na ulimwengu halisi. Lakini kupitia kwa dhana hii hatujaelezwa hasa kinachofanyiwa malighafi ya kazi ya fasihi. Ili kutimiza hilo, dhana nyengine imependekezwa; kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuchukuliwa kama muundo, kama mpangilio maalum. Kila kazi imepangwa kwa hali ya juu sana na viungo vyake vinategemeana hivi kwamba kazi kamilifu huwa ni mwafaka zaidi kuliko kiungo chake kimoja. Aristotle amelizungumzia swala hili hata ingawa anazingatia zaidi ploti. Aristotle (1975:29) anasema:
Chombo kizuri, kiwe kiumbe au kitu kizima kilichojengwa kwa vipande. Kazi ya fasihi yapaswa kutolewa kama kitu kimoja. Ploti, kama mithili ya kitendo, lazima imithilishe kitendo kimoja; na muungano wa vipande vya kitu kizima uwe hivi kwamba kipande kimoja kikiondolewa pale, kile kitu kizima hutengana. Kwani kipande ambacho hakitoi athari kiondolewapo, bila shaka si kipande halisi cha kizima.
Tukitizama fasihi kwa njia hii, tunatambua umoja na uwiano wa kila kazi unaoifanya ieleweke na iwe na muundo maalum. Hivyo basi kazi ya fasihi ni muundo wa vipande vinayopatana na kuhusiana ili kujenga kitu kimoja. Hivyo basi kipande kimoja cha kazi hiyo huwa hakina maana yoyote kivyake mpaka kihusishwe na vingine.

Kama ambavyo dhana ya ubunilizi hutusaidia kutofautisha fasihi na matukio halisi maishani, dhana ya muundo hutuwezesha kutofautisha fasihi na matumizi mengine ya lugha. Inatutolea ile hali ya usababishano, kwamba kazi ya fasihi ni utungo ulioundwa kwa visa vinavyowiana hivi kwamba kimoja hutangulia kingine. Pia, kisa kimoja hutokea ili kusababisha kingine na vyote vinahusiana kwa njia ambayo kimoja hakiwezi kueleweka bila kingine. Haya yote yanawezekana kupitia lugha inayotumiwa. Kwa hivyo katika muundo, tunazingatia jinsi lugha inavyotumiwa.

Nadharia ya Uhalisia-Nafsi
Kigezo kingine kinachotumiwa katika kuianisha fasihi ni kuiona fasihi ile kama zao la mtunzi binafsi. Fasihi kwa mtazamo huu huzingatia saikolojia na sifa za mtunzi huyo. Kigezo hiki kimezingatiwa hasa katika nadharia ya tathimini saikolojia . Ni wazi kwamba chanzo cha kazi ya sanaa ni yule anayeiumba, yaani mtunzi wake, na hivyo basi maelezo yanayopatana na hulka na maisha ya mtunzi yamezingatiwa kwa muda mrefu sana kama nguzo moja ya kueleza maana ya fasihi.  Waitifaki wa nadharia hii hushikilia kwamba kazi ya fasihi yaweza kuelezeka tu iwapo itazingatiwa kwa mkabala mmoja na maisha ya mtunzi wake. Hivyo basi fasihi huonekana kama kielelezo cha uhalisia wa maisha, jinsi yanvyotafsiriwa na nafsi ya mtu bila kujali ukweli kama unavyodhihiri kwa nje. Jinsi mtunzi anavyojieleza kupita kazi ya fasihi linakuwa jambo muhimu katika nadharia hii.

Katika mtizamo huu huu, fasihi imezingatiwa kama hisi; yaani ni kielelezo cha hisi za mtu binafsi (mtunzi). Jinsi mtu anavyoona na kuyahisi maisha linakuwa jambo la kuzingatiwa kama fasihi. Wataalam wa jadi wa fasihi kama vile Aristotle wanashikilia wazo hili hili kuhusu fasihi. Aristotle aliamini kwamba fasihi au ushairi hasa ni utanzu ambao kwao binadamu hutoa hisia zake za ndani kuhusu maisha. Hivyo basi ushairi ukawa ni kielezo cha uhalisia wa nafsi ya mtunzi, jambo ambalo limezingatiwa katika kueleza fasihi ni nini.
Hata wahakiki wanaozingatia nadharia ya tahakiki-saikolojia kama vile Sigmud Freud wanashikilia kwamba kazi ya fasihi ni kielezo cha ndoto na matamanio yasiotimizwa ya mtunzi pamoja na majaribio ya kutimiza matamanio yake. Kwa mtizamo huu, fasihi ni hisi, hisia na mataminio ya mtunzi; yaani maisha yake. Hapa ndipo twapata hata biografia zikichukuliwa kama kazi za fasihi.

Mtizamo kuu kuhusu fasihi haujapokelewa kwa mikono miwili na baadhi ya wataalam. Jefferson (1982:99) anasema:
Utunzi na usomaji wa fasihi hauna uhusiano wowote na nafsi halisi ya mtunzi na fasihi huwepo bila kutegemea mazingara halisi pamoja na hulka ya mtunzi.

Kwa hivyo, kazi ya fasihi haina uhusiano wowote na nafsi ya mtunzi wake. Anasema kuwa kazi ya fasihi hujisimamia yenyewe kama kazi ya fasihi na haihitaji kuhusishwa na mtunzi wake ili kueleweka ama kutungwa. Lakini hatuwezi kulitupilia mbali wazo hilo kwani kila kitendo cha kutunga hutokana na fikira, maoni, tajiriba, na hisia za mtunzi, jambo ambalo lina ubinafsi maalum unaodhihiri, japo kwa kiwango duni, hulka ya mtunzi huyo.
Nao Wellek na Warren (1949:78) wana maoni haya kuhusu mtizamo huo wa fasihi:
Wazo kwamba sanaa kwa ujumla ni uhalisia-nafsi unaotoa hisi na tajiriba za mtu, ni la kupotosha. Hata panapotekea uhusiano wa karibu sana kati ya sanaa na maisha ya mtunzi, hili lisichukuliwe kumaanisha kwamba sanaa ni mwigo wa maisha. Mtizamo huu husahau kwamba kazi ya sanaa ni kazi kivyake wala si kusanyiko la tajiriba za mtunzi.
Maoni ya wataalum hawa yanadhihirisha wazo la awali kwamba fasihi ni kazi inayojisimamia na iliyo na kaida zinazoitawala. Hivyo basi, tamthilia, riwaya au shairi huwa zinaongozwa na kutawaliwa na kaida za kifasihi zinazohusu kila utanzu. Tukichunguza mtizamo huu kuhusu fasihi twaona kwamba unapuuza baadhi ya hoja halisi za kimantiki. Kazi ya sanaa huenda ikawa si maisha halisi ya mtunzi bali ni maoni au mtazamo wake kuhusu maisha. Huenda ikawa pia ni kinyago cha kuficha nafsi yake halisi au huenda ikawa picha ya maisha anayotaka kuyakimbia. Isitoshe, tusisahau kwamba huenda tajiriba ya maisha halisi ya mtunzi ikawa tofauti na ile ya sanaa; yaani tajiriba halisi maishani hutazamwa kwa jinsi ambavyo zitafaa fasihi na huwa kwa kiasi fulani zimeongozwa na kuathiriwa na kaida za kisanaa zinazotawala kazi yake. Ama kweli kazi ya fasihi inayoorodhesha matukio kama yalivyo bila usanii si sanaa bali ni kumbukumbu au historia.

Hata hivyo hatuwezi kupuuza kabisa kigezo hiki kwani kinachangia katika kueleza fasihi ni nini. Lililo muhimu kutambua ni kwamba kigezo hicho hakiwezi kutumiwa peke yake kueleza fasihi ni nini. Ni lazima kihusishwe na vigezo vingine mbali mbali ili kutoa picha kamili na pana ya fasihi.

Nadharia ya Mguso
Mtizamo huitazama fasihi katika uhusiano wake na umma wake ambapo msisitizo unatiliwa mguso unaotolewa na kazi ya fasihi kwa hadhira yake. Kila kazi ya fasihi hulenga kwa njia moja au nyingine mtu au watu fulani (hadhira) hata kama hadhira hiyo ni nafsi ya mtunzi husika. Kazi ya fasihi hutoa mguzo wa aina fulani kwa hadhira ili ifikirie na kujiuliza maswali au hata kutoa funzo fulani.

Kwa kuunga mkono maoni haya, Vasquez, A.S (1973:113) anasema:
.... kazi ya sanaa huathiri watu na inachangia katika kuhimiza au kupuuza dhana zao, maazimio yao, hata maadili yao - ina msukumo wa kijamii ambao huathiri watu kwa nguvu zake za kihisia na kiitikadi.
Ama kwa hakika, hakuna anayebaki vile vile baada ya `kuguswa' na kazi ya halisi ya sanaa.

Kuna nyakati ambapo imependekezwa kwamba hadhira hutekwa kabisa na wahusika katika kazi ya fasihi mpaka hadhira hiyo ikajitambulisha na wahusika hao kiasi cha kupoteza utambulishi wake asilia, hata kama ni kwa muda tu. Hata Wellek na Warren (1949:102) wana maoni yayo hayo wasemapo:
Watu wamewahi kubadilisha mienendo yao katika maisha kwa kuathiriwa na wahusika wa kubuni katika fasihi.
Tunachokisisitiza hapa ni wazo lile lile kwamba kazi ya fasihi hutoa mguso kwa hadhira yake, na huu mguso ndio unaotumiwa kama kigezo cha kueleza maana ya fasihi. Ndiposa twapata wataalamu wengine wakisema kuwa fasihi ni kazi ya kufurahisha. Horace (1975:103) anasema “washairi hulenga kusaidia au kufurahisha msomaji, au kusema kile kinachopendeza na wakati huo huo kusema kinachofaa.”

Tatizo linalozuka katika mtazamo huu ni kwamba ni vigumu kusema kama kweli pamesababika au kutokea mguso wowote kwa hadhira baada ya kusikiza, kuona au kusoma kazi ya fasihi. Mguso aghalabu ni jambo la kihisia na kibinafsi na huwa vigumu sana kutathiminiwa. Isitoshe, yahitajika kupima na kutathimini kiwango cha mguso huo, kama upo, ili kupata hitimisho lenye mashiko. Jambo hili huenda likawa gumu sana kutimizwa. Lakini iwapo ni watu ambao tunawafahamu ni rahisi kuthibitisha kama wamebadili maoni au mienendo yao kuhusu jambo fulani ambalo limegusiwa katika kazi ya fasihi.

Baada ya kuorodhesha vigezo hivi mbali mbali vinavyotumiwa kueleza fasihi, pana jambo ambalo linadhihirika kila mara na katika kila kigezo -- kwamba fasihi ina uhusiano mkubwa na jamii, na hakuna fafanuzi moja inayoweza kusimamia kazi zote za fasihi, kila moja yategemea muktadha na dhamira ya mfafanuzi. Haya tuliyoyatoa hapa ni maongozi ambayo yanaweza kusaidia katika kuielewa fasihi kama dhana pana lakini iliyo na sura maalum zinazotambulika. Tungependa kupitia dhana hii ya fasihi na jamii kwa sababu, mbali na kuwa muhimu katika kazi yetu, dhana hii imetumiwa pia katika kueleza maana ya fasihi.

Fasihi na Jamii
Fasili nyingi za fasihi zimeegemea kuileza katika uhusiano wake na jamii. Fasili hizi zimeonyesha kwamba fasihi ni taasisi ya jamii na uhusiano wake na jamii hauwezi kupuuzwa. Mmoja wa wanaounga mkono dhana hii ni Escarpit, R (1974:4) anayesema kwamba:
Fasihi lazima ichukuliwe kama iliyo na uhusiano usiotatanika na maisha ya kijamii.
Fasihi ni taasisi ya kijamii, inayotumia lugha kama mtambo wake. Isitoshe, fasihi huwakilisha maisha. Maisha kwa upana wake huhusu uhalisi wa kijamii, hata ingawa ulimwengu halisi na hata ulimwengu wa ndani wa mtu binafsi ni mambo yanayoweza kuzingatiwa katika fasihi. Mbali na hayo twafahamu kwamba iwapo fasihi hulenga watu fulani, basi bila shaka hiyo fasihi yahusu jamii fulani lau sivyo hapana haja kutungia watu kazi isiyowahusu ndewe wala sikio.

Jambo jingine la kutaja hapa ni kwamba mtunzi mwenyewe ni mwanajamii kwa ambavyo ana nafasi na tabaka fulani katika jamii yake; yeye hutambuliwa na jamii kama mmoja wao. Hawezi kuepuka nafasi hiyo yake katika jamii wala hawezi kukwepa athari ya jumuiya katika utunzi wake kwani kama mtoto mchanga yeye anafundishwa maadili na itikadi za jamii yake ili kuweza kuenea katika jamii hiyo. Na kama ambavyo tumetaja tayari, mtunzi hulenga hadhira fulani hata iwe ndogo vipi.

Mara nyingi fasihi hutokana na uhusiano wa karibu sana na taasisi maalum za kijamii. Taasisi za kiuchumi, kisiasa, na kijamii zimekuwa na uhusiano mkubwa sana na utoaji wa fasihi na kila kazi ya fasihi kwa njia moja au nyengine, hudhihiri ukweli huu. Maendeleo na mabadiliko ya jamii yametokea kuwa maendeleo na mabadiliko ya fasihi hivi kwamba hatuwezi kutenganisha fasihi na jamii inamoibukia. Uhusiano huu unatokea kwa sababu pindi maisha ya jamii yabadilikapo, mielekeo, tamaduni na hata maadhili ya jamii hubadilika pia. Aidha, mabadiliko ya fasihi toka simulizi hadi andishi ni zao la mabadiliko katika maisha ya jamii ambapo taaluma ya kusoma na kuandika ilitokea. Kwa hivyo fasihi inalo jukumu kuu katika jamii ambalo sio la kibinafsi, bali ni la kijamii. Katika kuiunga mkono kauli hii, Wellek na Werren (1949:95) wanasema kwamba:
Uhusiano kati ya fasihi na jamii hujadiliwa kwa kuanza na kaulo aliyoitoa De Bonald kwamba `fasihi ni kielelezo cha jamii'.

Kwa hivyo ni muhimu kuichukulia fasihi kama zao la jamii ambalo pia huathiri na kuathiriwa na jamii.

Hata katika nyingi za tahakiki za fasihi ambazo twaweza kuziita za kijamii (kama za Ki-marx) pamesisitizwa kauli kwamba mtunzi anapaswa kuendeleza maisha ya wakati wake kwa ujumla wake; kwamba anapaswa kuwa kiwakilishi cha wakati wake na jamii yake. Kwa maoni ya waitifaki wa tahakiki hizi, `uwakilishi' huelekea kumaanisha kuwa mtunzi anapaswa kutambua na kuona hali halisi za maisha katika jamii yake na kuzizingatia katika utunzi wake. Maoni ya Hegel na Taine katika Wellek na Warren (1949:95) ni mfano unaochangia zaidi kauli hii wanaposema:
Katika uhakiki wa Kihegel na hata ule wa Taine, utukufu wa kijamii na wa kihistoria huenda sambamba na utukufu wa kisanaa. Msanii huendeleza ukweli, na huo ukweli ni wa kijamii na kihistoria.
Tunaloweza kuongeza ni kwamba pana tatizo linalokumba juhudi yoyote ya kujaribu kutenganisha fasihi na jamii kwani fasihi huathiriwa na mandhari ya kijamii pamoja na mabadiliko na maendeleo yake. Isitoshe, mtunzi ni mwanajamii anayetumia lugha ya jamii kutunga kazi yake ili kuwafifikia wanajamii husika. Ukweli huu wanaogusia waandishi hawa utategemea mtizamo, matarajio, na tajiriba za anayehusika kwani hali mbali mbali katika jamii hutoa maana mbali mbali kwa watu mbali mbali hata kama ni wa jamii moja. Hivyo basi ukweli hubainika tu kimuktadha.

Wale wanaosisitiza kigezo cha fasihi na jamii katika kuieleza fasihi, wametoa kauli kwamba pana aina mbali mbali za fasihi ambazo zinachukuana na jamii mbalimbali. Dhana kama vile fasihi ya kirusi, fasihi ya kiafrika, fasihi ya kiingereza n.k. ni baadhi ya mifano ya kazi za fasihi zinazohusishwa na jamii fulani. Fasihi kama hizi hulenga jamii fulani pana zenye kaida na maadili yanayopatana katika muundo wa kijumla kwani katika jamii hizo huwa kuna vijamii vidogo vidogo. Kwa mfano katika fasihi ya Kiafrika pana fasihi ya jamii ya nchi mbali mbali ambazo zimeibuka kihistoria kwa jinsi maalum ambao ni tofauti na ya nchi nyengineyo. Na katika nchi hizo pana vijamii vingine vidogo vidogo vinavyobainishwa na lugha, mazingira, na itikadi. Hivyo kutaja kwamba pana fasihi ya kirusi ni kutoa kauli ya kijumla tu. Vile vile pana fasihi zinazochukuana na mifumo mbali mbali ya maendeleo ya kijamii kama vile fasihi ya kibwanyenye, fasihi ya kisosholisti, fasihi ya kikapitolisti n.k.

Ama kwa hakika mojawapo ya majukumu ya fasihi ni kule kuihifadhi historia ya jamii husika. Yaani kwa kuitazama kazi ya fasihi twaweza kupata picha maalum ya historia ya jamii husika. Kwa mfano katika fasihi ya kiswahili twaweza kupata vipindi maalum vya kihistoria. Dunia Mti Mkavu (Said A. Mohamed) ni mfano wa kazi inayoonyesha historia ya unyonyaji na unyanyasaji wa mufumo wa ukoloni, Mashetani (Ebrahim Hussein) ni mfano wa Kipindi cha Ukoloni-Mamboleo, na utenzi wa Al-Inkishafi (Sayyid Nassir) ni kielelezo cha historia ya Mji wa Pate. Hivyo basi twaona kwamba kauli kuwa fasihi ina uhusiano mkubwa na jamii ni dhana yenye mashiko sana.

Hata hivyo hatulengi kusema kwamba kazi ya fasihi ni hitoria kwa kule kuhitajika kutoa picha halisi ya maisha ya wakati husika, kwani japo mada ni matukio halisi ya kihistoria, namna ya kusawiri mada hizo na matini maalum (kati ya mengi) yaliyozingatiwa, ndiyo yaibainisha kama kazi ya fasihi. Maoni yaliyotolewa hapa ni mwongozo wa kuitazama fasihi katika vigezo ambavyo bila shaka huathiri fasihi. Iwapo tutakubali kwamba kazi ya fasihi si amali ya mtu binafsi, basi tutakuwa tayari tumeonyesha kwamba fasihi na jamii ni vitu visivyotengana. Na hata pakitokea kwamba maisha ya mtu binafsi yametumiwa kama nguzo ya kutunga kazi ya fasihi, hatuwezi kusahau kwamba tajiriba zake zimepaliliwa na maisha yake kama mwanajamii, awe anachukua au kukiuka maadili na matarajio ya jamii hiyo.

Hitimisho
Baada ya kutazama mitazamo na vigezo mbalimbali vilivyotumiwa katika kueleza fasihi ni nini, twaweza kutoa muhtasari wa kauli muhimu zilizotokea ili kupata fasili ya fasihi. Baadhi ya maoni yaliyotolewa kuhusu fasihi, yameathiriwa sana na historia. Kwamba matarajio na majukumu yaliyowekewa fasihi yanabadilikabadilika ili kuchukuana na mabadiliko ya kihistoria. Kwa mfano kule kuiona fasihi kama amali ya jamii zenye taaluma ya maandishi lilikuwa tokeo la kiburi cha wanajamii waliotaka kutenga jamii yao `iliyostaarabika' na jamii za `kishenzi' ambazo hazikuwa na ujuzi wa kusoma na kuandika. Vile vile, kule kuanza kuitazama fasihi kama uhalisia-nafsi wa mtunzi ni matokeo ya juhudi ya binadamu kuingia katika ubinafsi na upweke ulioletwa na mabadiliko katika mkondo wa maisha. Hapo awali, wanajamii waliishi kwa pamoja na kushirikiana, lakini baada ya idadi ya watu kuongezeka pamoja na jamii kupiga hatua katika sayansi, dhana ya umoja katika jamii ilitoweka na badala yake pakaingia ubinafsi. Hivyo basi badala ya mtunzi kulenga mambo yanayohusu jamii nzima katika kazi yake, akaanza kuitumia fasihi kama chombo cha kuendeleza maisha yake ya kibinafsi na kuondoa upweke.

Kwa upande mwingine twapata katika nyakati za umwinyi na ukoloni (ambapo watu wachache waliwakalia walio wengi katika jamii) fasihi ilitumiwa kuburidisha watawala na wenye nguvu na ilipata kuhimizwa sana kwa kutumia hizo nguvu. Bila shaka hili halikufaa kwani fasihi haibagui katika athari zake. Ndiposa palitokea mawazo kwamba fasihi yapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha ya wakati wake. Ikawa basi katika ukandamizi huo palizuka fasihi ya upinzani ya walio wengi kupinga unyanyasaji na dhuluma.

Kwa hivyo, mawazo yote yaliyotokea kuhusu `fasihi ni nini' hayakutokea kwa sadfa bali ni kwa kufuatana na mabadiliko ya maisha kihistoria. Jambo jingine muhimu ambalo tungelitaja hapa ni kwamba baadhi ya kazi nyingi za kufasili maana ya fasihi zimeathiriwa sana na maoni ya wasomi wa kimagharibi na wasomi wengi wa Kiafrika kwa mfano huwa wanaifasili fasihi mara nyingi kwa kulenga maoni ya hao wasomi wa kimagharibi. Nayo maoni ya wasomi wa kimagharibi wameegemeza maoni yao kuhusu fasihi na jamii kwa jumla katika falsafa na maoni ya wataalamu mbali mbali.

Mikutano kati ya jamii mbali mbali za kilimwengu iliyosababishwa na usafiri, biashara, na utawala (hususa ukoloni) na pia mabadiliko ya kijamii kihistoria yalichochea fikira za wasomi wengi hasa wa kimagharibi ambao walivutiwa na swala la mabadiliko ya kijamii. Maoni ya kuendelea kwa jamii toka hali ya duni (ushenzi) hadi ya juu (ustaarabu) iliyofafanuliwa na wasomi kama vile Darwin iliwatia moyo sana wasomi wa kimagharibi ambao walitaka kuchunguza hali hiyo kwa kuzitafiti jamii ambazo ‘hazikuwa zimeendelea.’ Nadharia hii ya Darwin ilidai kwamba jamii hizi zitaendelea na kufikia kiwango hicho cha juu na hivyo basi wasomi walipapia kuzitafiti jamii hizi duni kabla ya kupata maendeleo.

Masomo kama vile anthropolojia yalizuka kuzingatia hali hiyo ya utafiti ambao ulizingatia kuorodhesha maisha ya watu wa jamii za hali ya chini kabla hayajaangamizwa na maendeleo. Ndiposa palizuka utafiti linganishi ambao ulitumia umagharibi kama kioo cha kuzitazama jamii nyinginezo hasa za Kiafrika, Kiesia, na za Kimarekani asilia. Hivyo basi utafiti katika karne ya kumi na tisa uliegemea zaidi jamii hizo ambazo zilionekana kuwa na maisha ya hali ya chini (ama yaliyo karibu na ya wanyama). Maswala muhimu wakati huo yakawa ni kutazama tofauti kati ya ujumuia na ubinafsi, dini na ukosefu wa dini, usosholisti na ukapitolisti, na himaya za kifalme na za kidemokrasia ambayo yaliadhiriwa sana na maoni ya wasomi wa kisosholojia kama vile Emile Durkheim na wa ulimbikaji mali kama vile Karl Marx.

Hata wasomi wa Kiafrika waliendeleza kauli hii kwa kukimbia kurekodi mila na tamaduni zao ambazo waliziona zinaadimika na nafasi zao kuchukuliwa na ‘maendeleo’ ya kimagharibi. Haya yote yalidhihirisha msimamo wa wasomi hawa wote kuhusu jamii na utamaduni. Ni wazi kwamba walichukulia utamaduni kuwa kitu finyu ambacho chaweza kuopolewa na kuhifadhiwa. Mwelekeo huo ni hatari kwani unapuuza hali kwamba watu daima hubadili maoni, maadili, na kaida zao ili kuchukuana na mazingira yao ambayo hugeuka kila wakati. Hivyo ndivyo ilivyokuwa na usomi kuhusu fasihi.

Hata hivyo tukirejelea vigezo tulivyotumia kuieleza fasihi hapo juu, twapata hoja kuu zifuatazo zikijitokeza:
·         Fasihi hutegemea jamii.
·         Fasihi hutumia maneno kama njia ya kuwaisilisha mambo yake
·         Fasihi huhusu maisha ya jamii husika lakini si kwa kutoa picha ya moja kwa moja kama historia.
·         Fasihi hulenga hadhira fulani ambayo huiathiri.
·         Fasihi hutawaliwa na kaida na masharti ya kisanaa.
·         Mtunzi hutumia ubunifu wake katika kuitunga kazi ya fasihi.

Kwa hivyo kwa kutumia hoja hizi tutajaribu kutoa fasili ya dhana ya fasihi. Kwa maoni yetu, fasihi ni sanaa inayotumia ishara (maneno au matendo) kutoa picha halisi ya maisha kwa njia bunifu na inayofuata mpangilio maalum na lugha ya kifasaha ili kuiathiri hadhira husika. Fasili hii inadhamiria kuchukua tanzu zote za fasihi (fasihi andishi na simulizi). Hata hivyo twafahamu kwamba sio kila kazi ya fasihi hutimiza viwango hivyo tulivyovipitia. Vile vile sio kila kazi ya fasihi huratibiwa kwa kiwango kimoja cha ubora, pana kazi nzuri kisanaa, kimaudhui au vyote viwili. Vigezo tulivyovitoa hapo juu ni mwongozo kwa mhakiki na mwanafunzi wa fasihi anayekabiliana na swala la fasihi na uhakiki.

Kwa kuhitimisha tutataja kwamba mitazamo na vigezo mbali mbali tulivyovitaja kuhusu kueleza fasihi vyaweza kutumiwa katika baadhi ya nadharia za uhakiki wa kazi za fasihi. Kwamba iwapo kigezo fulani kitatumiwa kueleza fasihi, basi kigezo hicho hicho kitatumiwa kuihakiki fasihi. Kwa mfano iwapo fasihi imeelezwa kama uhalisia nafsi, basi katika uhakiki wa kazi hiyo maswala ya maisha na saikojia ya mtunzi yatatiliwa maanani.

Tungependa kukiri kwamba dhana ya fasihi inazua utata mwingi sana na kamwe hatudai tumetatua utata huo. Pamekuwepo na pataendelea kuwepo misingi mbali mbali ya kueleza fasihi kulingana na msisitizo anaochagua mhusika. Pana wale wanaochagua mtindo wa fasihi peke yake. Pana wale wanaochagua maudhui ya fasihi peke yake. Pana wale wanaochanganya vyote viwili; na wote huwa wana haki ya kufanya vile na kujihimili kwa kauli zao mbali mbali.

DHANA ZA FASIHI
1.       Fasihi andishi: ni fasihi inayohifadhiwa katika maandishi (mathalani novella, riwaya, hadithi fupi, mashairi, tamthilila, insha na tawasifu)
2.       Fasihi ashiki: ni fasihi inayojihusisha na mambo ya kimapenzi. Huweza kuwa na lugha inayopuuza kaida na mbeko za matumizi ya lugha
3.       Fasihi badili: ni fasihi ambayo haipo katika mkondo huu. Huweza kupinga kaida zilizopo
4.       Fasihi chapwa: ni kazi ambazo hazina uzito wa kimaudhui au kimtindo na hukusudiwa kuwasisimua wasomaji kwa visa visivyoonyesha ufundi mkubwa wa utunzi
5.       Fasihi elekezi/ fundishi: ni fasihi iliyoandikwa kimsingi kuelimisha na kuelekeza kwenye njia maalumu kama vile dini au falsafa
6.       Fasihi kale/ kongwe: ni fasihi ambayo imekuwako tangu kale nab ado ina mchango na umuhimu mkubwa katika jamii husika
7.       Fasihi leo: ni fasihi ya kipindi kilichopo iliyo chini ya mfumo wa kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na kisiasa
8.       Fasihi linganishi: ni uchunguzi wa maandishi ya wakati mmoja na aina moja na katika lugha mbalimbali ili kumulika sifa zinazoyahusisha, kuangalia matapo mbalimbali, maendeleo au nadharia za uhakiki
9.       Fasihi pendwa: ni fasihi inayopokezwa kwa masimulizi
10.   Fasihi simulizi: ni fasihi inayopokezwa kwa masimulizi
11.   Fasihi ungamo: ni fasihi ambamo mhusika fulani huyakubali makosa aliyoyafanya nap engine kutubu
12.   Fasihi ya kibaadaukoloni: ni fasihi ihusishwayo na maandishi ya wanaochimbukia nchi zilizokuwa chini ya utawala wa kikoloni
13.   Fasihi ya kibwanyenye: ni fasihi ijihusishayo na tabaka la mabwanyenye wasiojihusisha na (shida za) wanyonge
14.   Fasihi ya kibwege/ kidhanaishi: ni fasihi ambayo wahusika wake hupambana na maisha wanayoyaona hayana maana hasa kwa kuwa hapaelekei kuwa na nguvu inayoweza kuyaathiri au kuyapinga. Hujikita katika udhanaishi
15.   Fasihi ya kidini: ni fasihi yenye maudhui ya kidini
16.   Fasihi ya kifomula: ni fasihi inayotambulika kwa matumizi maalumu ya mbinu mbalimbali. Fomula hizi ni fomula funguzi na fomula kimalizio
17.   Fasihi ya kimakimbizi: ni fasihi inayojitenga na maswala ya jamii halisi kimakusudi na kujihusisha na maswala yasiyoelekea kuwa muhimu
18.   Fasihi ya kinjozi/ kifantasia: hujengwa kwenye msingi wa mambo yasiyoeleweka
19.   Fasihi ya kipembezoni: ni fasihi inayozuka katika nchi zilizotawaliwa na mkoloni na huhusisha lugha ya wakoloni. Pia ni fasihi ya jamii za kipembezoni hasa katika mazingira ambapo kuna tamaduni nyingine kuu
20.   Fasihi ya kitabiri: ni fasihi inayohusu jamii zinazohusiana kilugha au kitamadunni
21.   Fasihi ya watoto: ni fasihi iliyoandikiwa watoto

UMUHIMU WA FASIHI
1.       Kuelimisha jamii kuhusu vipengele mbalimbali vya maisha
2.       Kuelekeza mtu
3.       Kuburudisha, kufurahisha na  kuchangamsha kwa kujihusisha na viungo vya mwili kuliko akili
4.       Kudhalilisha kwa kutumika kama silaha ya kujikinga dhidi ya adui
5.       Kumkomboa mnyonge kutoka dhuluma. Hutoa wanajamii magofu ya pazia machoni ili waweze kuyasawiri na kuyaelewa matatizo yao  kwa macho ya ndani na kuwaonyesha mbinu za kujikomboa
6.       Kukuza na kuendeleza kupawa cha lugha hasa kwa upana na uzito wake kwa sababu huzingatia vipengele vya lugha na kuviimarisha
7.       Kuendeleza historia  kwani ni bohari ya kuhifadhi amali za jamii na kihistoria
8.       Kufichua uozo wa jamii na kuwapa mwongozo wanaokandamizwa
9.       Kuhifadhi amali na desturi za jamii kwa kuzirithisha kwa vizazi vingine
10.   Kuzindua na kukomaza mtu kujua mazingira na utamaduni
11.   Kuadilisha jamii
12.   Kufanikisha ushirikiano  miongoni mwa makundi mbalimbali (kabila, umri, jinsia na tabaka) inapochanganuliwa
13.   Kuunganisha vizazi kwa kutambua mnaisha ya vizazi vilivyotangulia yalivyokuwa. Aidha huweza kujinasibisha nacho, hasa kunapokua na wiano wa amali, mwelekeo na maadili.

TANZU ZA FASIHI
Kigezo muhimu cha kuainisha fasihi ni vile msanii anavyoupitisha ujumbe wake. Mintarafu ya hii, tuna aina mbili za fasihi – fasihi andishi na fasihi simulizi. Fasihi andishi hutegemea maandishi kuupitisha ujumbe wake ilhali fasihi simulizi hupitisha ujumbe wake kivitendo na/au kikalima

FASIHI SIMULIZI
UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI
1.       Kuburudisha na kuchangamsha
2.       Kurithisha na kufahamisha kuhusu utamaduni, desturi , mila na itikadi za jamii
3.       Kusaidia kujielewa kwa kutufafanulia tulikotoka, historia yetu, asili yetu, mazingira yetu na kazi zetu
4.       Kunoa akili kwa kuwapa watu ujuzi wa kuwaza na kutatua matatizo ya jamii
5.       Kuhifadhi utamaduni kwa kuonyesha vile utamaduni wa kigeni ulivyoathiri jamii
6.       Kuimarisha kipawa cha lugha kwa kuwawezesha kukuza ukakamavu wa kujieleza mbele ya hadhira
7.       Kukuza umoja, ushirikiano na uhusiano bora kati ya wanajamii
8.       Kuielekeza jamii
9.       Kuunganisha vizazi vya jamii
10.   Kuhamasisha uzalendo na ari ya kujikomboa kutoka kwa walowezi
11.   Kuwanoa vijana akili

KIPIMWACHO KATIKA FASIHI SIMULIZI
Katika tathmini ya Fasihi Simulizi, mtahiniwa anatakiwa:
1.       Kulielewa swali na kulifasiri inavyotakiwa
2.       Kuainisha tanzu na vipera vyake
3.       Kutoa vijelezi mwafaka vya vipera
4.       Kufafanua dhima na umuhimu wa vipera hivi
5.       Kutoa mfano wa vipera hivi
6.       Kuhakiki vipera hivi vya Fasihi Simulizi kimaudhui, kimuundo, kimtindo na wahusika
7.       Kulinganisha na kulinganua vipera mbalimbali
8.       Kufafanua mafunzo na maadili yanayojitokeza katika kipera husika
9.       Kubainisha tukio na mkutadha wa utendaji wa kipera
10.   Kuonyesha nafasi ya vipera katika ulimwengu wa sasa
11.   Kukuza uwezo wa kukusanya na kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi

SABABU ZA KUPUNGUA KWA FASIHI SIMULIZI
1.       Uvumbuzi wa maandishi. Awali Fasihi Simulizi ndiyo iliyokuwa sanaa ya pekee ya lugha. Kupitia kwayo wanajamii walijifurahisha na kuhifadhi mila na tamaduni zao. Mengi sasa huhifadhiwa katika maandishi
2.       Washindani badala. Awali, watoto walijumuika kusimuliwa hadithi au vitendawili. Siku hizi pumbao la watoto halitokani na masimulizi kwa sababu wametekwa na vitumeme vya kila nui. Fasihi Andishi, redio, runinga, tarakilishi, mtandao, pataninga na vifaa vinginevyo hutumiwa siku hizi kama njia badala za kujipumbaza.
3.       Mapisi. Watoto wa sasa hushughulika mno na elimu ya vitabu kuliko ya mapokeo
4.       Mwingiliano na mtagusano wa jamii mbalimbali. Mtagusano wa watu wa jamii mbalimbali umepunguza uhalisia wa Fasihi Simulizi. Vijana hawawezi kujieleza kwa lugha moja. Kumeibuka jamii isiyo na lugha wala utamaduni imara. Wamerithi mchanganyiko wa mawazo kadhaa. Labda tuuite utamaduni mseto au chotara.
5.       Uhakiki wa Fasihi Simulizi. Ulinganishi wa Fasihi Simulizi za jamii mbalimbali hudumaza tanzu hizi. Tamasha za muziki na maigizo shuleni na vyuo huwa zimetengwa na hali halisi ya utendaji wa tanzu hizi
6.       Mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu hutilia mkazo masomo mengine huku Fasihi Simulizi ikipuuzwa

YA KUZINGATIA ILI FASIHI SIMULIZI IENDELEE KUWEPO
1.       Kusisitiza utafiti wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi
2.       Kuifundisha Fasihi Simulizi shuleni na taasisi nyinginezo
3.       Kuhimiza uhifadhi wa Fasihi Simulizi
4.       Kuhakikisha lugha za kienyeji hazifi
5.       Kupambana na lugha za kikoloni ili wanajamii wasidharau Fasihi Simulizi

NADHARIA ZA FASIHI SIMULIZI

Nadharia ni sayansi ya kanuni za jumla na mikabala fulani itumiwayo kuchunguza swala fulani. Wataalamu wa Fasihi Simulizi wamazuka na nadharia kadha za kueleza asili, chanzo , ukuaji na ueneaji wa Fasihi Simulizi

1.      Ubadilikaji
Hii ni nadharia yenye historia ndefu na inategemezwa kwenye mawazo ya Charles Darwin. Nadharia hii hudai kuwa sanaa ya usemaji ilizuka tu katika harakati za maingiliano ya binadamu ya mazingira yake. Inachukulia kuwapo kwa usawa fulani katika maisha ya binadamu hivi kwamba kuna sifa fulani zinazopatikana katika hatua fulani za kila jamii. Sanaa hubadilika kutoka hatua ya chini (ghafi) hadi nyingine ya juu kadri wakati unavyobadilika.

2.      Msambao
Kiini cha nadharia hii ni fikira kuwa chochote kinachopatikana kina chanzo chake. Wanaoifuata husema kuwa sifa fulani za Fasihi Simulizi huwa na chanzo maalumu. Vyanzo hivyo ni pale hadithi ilipoibuka kabla ya kusambaa na kuenea sehemu mbalimbali. Nadharia hii hutumiwa kueleza sababu za kuwako mfanano fulani wa sifa za Fasihi Simulizi za jamii mbalimbali. Mweneo wa Fasihi Simulizi unachuchiwa na kuwako kwa tofauti za kihistoria au ukuruba wa jamii filani. Mahusiano ya karibu yanaathiri misuko, wahusika, visa, mada na matendo ya Fasihi Simulizi.

3.      Uamilifu
Huangalia Fasihi Simulizi kwa mujibu wa utendakazi wake. Huangalia mahusiano ya haja za jamii husika na jinsi yanavyiridhisha na kudumisha mfumo wa jamii hiyo. Mtazamo huu huchukuliwa kuwako kwa amali au sifa fulani za Fasihi Simulizi kunatekeleza malengo mahususi katika jamii hiyo. Kwa mujibu wa nadharia hii, Fasihi Simulizi inadhamiriwa kuhifadhi na kidukisha amali za jamii

4.      Odondosinafsi
Pia huitwa saikolojia changanuzi. Ni imani kuwa binadamu wote wana sifa sawa kwa kuwa wana muundo sawa wa akili. Kwa hivyo matendo ya binadamu yanaweza kufanana ingawa wametengana kihistoria, kijamii na kijografia. Hii ndiyo sababu Fasihi Simulizi za jamii mbalimbali zina uhusiano

SIFA BAINIFU ZA FASIHI SIMULIZI

1.       Husambazwa kikalima
2.       Huwa na hadhira mahususi iliyo hai
3.       Huwa na wakati na mahali maalumu pa uwasilishaji
4.       Huwa na fomula ya kiada ya kuanza na kumaliza
5.       Hulenga utendaji kunaoifanya hai
6.       Mtunzi asiyejulikana bali ni mali ya jamii
7.       Hubadilika kulingana na wakati
8.       Wahusika wa aina mbalimbali
9.       Huwa na vipera vingi
10.   Hutungwa kila wakati
11.   Msimuliza ndiye mhusika wa kati
12.   Ala zake kuu ni sauti, mdomo na ishara za mwili

TOFAUTI KATI YA FASIHI SIMULIZI NA FASIHI ANDISHI

Fasihi Simulizi
Fasihi Andishi
Mwanzo wake huwa masimulizi
Mwanzo wake huwa maandishi
Huwasilishwa kupitia mdomo na vitendo
Huwasilishwa kupitia maandishi
Husambazwa kupitia mdomo na vitendo
Husambazwa kupitia maandishi
Huhifadhiwa akilini mwa wanajamii
Huhifadhiwa vitabuni
Hubadilika inapowasilishwa kupitia ufaraguzi
Haibadiliki
Ni mali ya jamii
Ni mali ya mwandishi
Mtunzi hajulikani
Mtunzi anajulikana
Baadhi yake huzuka papo hapo
Huhitaji muda kutunga
Ina muundo rahisi kufuatika (muundo msago)
Ina muundo mgumu kufuatika (muundo kioo)
Uzuri wake hutegemea ubingwa wa fanani
Uzuri wake hutegemea ubingwa wa mwandishi
Ni rahisi kwa baadhi ya sifa zake kupotea inapopokezwa
Sifa zake hazipotei
Ina wahusika wengi tofauti
Ina wahusika wachache maalumu aghalabu binadamu
Hadhira tendi inayoshiriki moja kwa moja hivyo kuathiri kazi nzima
Hadhira tuli iliyojitenga na isiyochangia moja kwa moja
Fanani anaweza kufahamu mawazo ya hadhira yake papo hapo na kuubadilisha uwasilishi wake unapolazimu
Msanii hawezi kujua maoni ya hadhira hadi baada ya muda kupita na hivyo hatabadilisha chochote wakati huo
Ni kongwe kwani ilianza tu lugha ilipoanza
Ni change. Ilianza na uvumbuzi wa maandishi
Ina tanzu nyingi
Ina tanzu chache
Inahusu visa vya kubuni na vya kihistoria
Inahusu visa vya uhalisia wa maisha
Si lazima fanani au hadhira wajue kusoma
Ni lazima msanii na hadhira wajue kusoma
Ina mwanzo na mwisho maalumu
Huwa na mianso na miishio mbalimbali
Hutegemea viambato vingine kama mavazi, maigizo na ishara za uso ili kukamilika
Lugha ndiyo nyenzo kuu
Huwasilishwa wakati na mahali maalumu
Husomwa popote
Huwa njia ya pekee ya kupitisha maarifa
Hupatikana kwa urahisi bila gharama
Hutumia shadda, mahadhi na ishara za mwili kuibua athari
Hutumia tamathali za semi kuibua athari
Kiungo muhimu katika mapokezi ni masikio
Kiungo muhimu katika mapokezi ni macho

Licha ya tofauti hizi, tanzu hizi mbili hufanana kwa kiasi fulani:
1.       Hutokana na jamii halisia
2.       Huwa na majukumu sawa
3.       Hulenga hadhira maalumu au hadhira mseto
4.       Hubaini imani, falsafa na mielekeo ya jamii

TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
Utanzu ni sehemu inayojumuisha tungo zote zenye sifa pambanuzi za kimuundo na mbinu za uwasilishaji zinazofanana. Hivyo basi, utanzu ni sehemu kubwa ambayo ndani yake kuna aina mbalimbali za maumbo ya fasihi yanayotofautiana. Fasihi Simulizi hugawanyika katika tanzu mbalimbali kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:

1.       Aina ya lugha iliyotumiwa – ni lugha nathari au ni lugha ya kishairi? Ni ya mfululizo au ni ya mazungumzo?
2.       Muundo
3.       Mada inayoshughulikiwa

Mintarafu ya sifa hizi tuna tanzu zifuatazo

HADITHI
MAIGIZO
NUDHUMU
SEMI
Nyimbo
Shairi
Kisasili
Mivigha
Bembea
Maghani simulizi
·         Rara
·         Tendi
Methali
Ngano za usuli
Ngomezi
Mbolezi
Vitanza ndimi
Hurafa
Ulumbi
Uchombezi
Misimu
Ngano za mazimwi
Utani
Nyiso
Sifo
·         Pembezi
·         Tondozi
·         Majigambo
Utani
Mtanziko
Mazungumzo
Hodiya
Nahau
Migani
Majigambo
Ngero
Misemo
Hekaya
Michezo ya jukwaani
Jadiya
Lakabu
Soga
Uramali
Kimai
Ngonjera
·         Malumbano
·         Ya kisemezano
Mafumbo
Tarihi
Tohara
Kongozi
Mizungu
Mbazi
Mawaidha
Sifo
Vitendawili
Istiara
Tambiko
Tumbuizo
Vigani vya watoto
Tashbihi
Mchapo

Kasida

Shirikina
Kudhubahi
Wawe
Tanakali za sauti
Shajara
Nyimbo za siasa
Takriri za maana
Kumbukumbu
Nyimbo za vita
Masaguo

Nyimbo za watoto

Nyimbo za uwindaji

16 comments:

  1. hewalla.kazi murwa ajabu..shime wenzangu

    ReplyDelete
  2. Replies
    1. Uhalisi ni mojawapo ya nadharia katika uchunguzi wa fasihi inayoegemea hali halisi ya maisha yalivyo katika jamii.

      Delete
  3. Kazi njema sana hii Mwanazuoni mwenzangu!
    Kuwemo humu inawafaa wengi sana!

    ReplyDelete
  4. jadili chanzo na chimbuko laubunifu wa maandishi

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ubunifu katika sanaa hutegemea nadharia mbalimbali. Shughli (amali) za jamii huchangia kukuza ubunifu wa maandishi

      Delete
  5. Replies
    1. Miviga si nadharia bali ni kipera katika safihi kinajchohusishwa na utanzu wa maigizo. kinahusu sherehe zinazofanywa katika kipindi mahususi na kinaandamana na shughuli fulani kama vile tohara, kutambika n.k.

      Delete